Wb/sw/Mtaguso II wa Vatikano

< Wb‎ | sw
Wb > sw > Mtaguso II wa Vatikano

MTAGUSO II WA VATIKANO

MALENGO YA MTAGUSO WA PILI WA VATIKANO edit

Muda mfupi baada ya kuchaguliwa papa mwenye heri Yohane XXIII alitangaza uamuzi wake wa kuitisha mtaguso mkuu akiamini kwamba utaweza kuandaa na kusababisha ustawi mpya wa maisha ya Kanisa. Lengo kuu la mtaguso lilikuwa kuliamsha Kanisa likumbuke wito wake na kwa kujifanya upya kwa ndani lipate msukumo mpya wa kimisionari ili kuwatangazia watu wote ujumbe wa milele wa wokovu, amani na umoja.

Tangazo hilo lilitolewa tarehe 25-1-1959. Baada ya maandalizi mtaguso wa pili wa Vatikano ulifunguliwa tarehe 11-10-1962. Vikao vinne vikafanyika mpaka ulipofungwa tarehe 8-12-1965. Kila kikao kilianza Oktoba na kumalizika Desemba ya miaka hiyo.

Kwa kuwa Yohane XXIII alifariki tarehe 2-6-1963, vikao vitatu vya mwisho viliongozwa na mwandamizi wake, Paulo VI, na hati zote kumi na sita zikatolewa chini yake pia kwa kupigiwa kura ya ndiyo karibu kwa kauli moja. Maaskofu na wakuu wa mashirika kadhaa wenye haki ya kupiga kura walikuwa kama elfu tatu, wakiwakilisha karibu Kanisa lote duniani, isipokuwa nchi zile zenye kuwadhulumu Wakristo.



ORODHA YA HATI 16 ZA MTAGUSO edit

HADHI

JINA LA KILATINI 
KIFUPISHO 
YAHUSUYO 
TAREHE 

KATIBA

1.        Sacrosanctum Concilium
SC
Liturujia takatifu
4-12-1963

2. Lumen Gentium

LG
Kanisa
21-11-1964

3. Dei Verbum

DV
Ufunuo wa Kimungu
18-11-1965

4. Gaudium et Spes

GS
Kanisa katika ulimwengu wa kisasa
7-12-1965

MAAGIZO

1.        Inter Mirifica
IM
Vyombo vya upashanaji habari
4-12-1963

2. Orientalium Ecclesiarum

OE
Makanisa katoliki ya Mashariki
21-11-1964

3. Unitatis Redintegratio

UR
Ekumeni
21-11-1964

4. Christus Dominus

CD
Huduma ya kichungaji ya maaskofu
28-10-1965

5. Perfectae Caritatis

PC
Kurekebisha upya maisha ya kitawa
28-10-1965

6. Optatam Totius

OT
Malezi ya kipadri
28-10-1965

7. Apostolicam Actuositatem

AA
Utume wa walei
18-11-1965

8. Ad Gentes

AG
Utendaji wa kimisheni wa Kanisa
7-12-1965

9. Presbyterorum Ordinis

PO
Huduma na maisha ya kipadri
7-12-1965

MATAMKO

1.        Gravissimum Educationis
GE
Malezi ya Kikristo
28-10-1965

2. Nostra Aetate

NA
Uhusiano wa Kanisa na dini zisizo za Kikristo
28-10-1965

3. Dignitatis Humanae

DH
Uhuru wa dini
7-12-1965



MAPOKEZI YA MTAGUSO edit

Wakristo walio wengi walipokea kazi ya mtaguso kwa mikono miwili, na wengi nje ya Kanisa pia waliridhika sana. Kutokana nao yamepatikana matunda mengi, lakini zimejitokeza hata kasoro na shida kwa sababu mbalimbali, hasa kwa kutoelewa wala kutotekeleza sawasawa maagizo yake. Kwa vyovyote hatuwezi kusema yote yaliyotokea baada ya mtaguso yamesababishwa nao, k.mf. maovu yaliyofanywa na baadhi ya mapadri hayamo kabisa.

Pamoja na upinzani wa wazi wa mifumo kadhaa ya kisiasa (ukomunisti na ubepari) na matapo mengine (Wamasoni n.k.) dhidi ya Kanisa, hali ya jumla ya ulimwengu inazidi kuelekea anasa na kuabudu utajiri hata kuzima maisha ya Kiroho. Hivyo ni vigumu kufanikisha mtaguso.

Hata ndani ya Kanisa wengi wamesoma hati zake kijuujuu, wakishikilia upande mmoja na kutojali wa pili. Wengine wamevunjika moyo kuona utekelezaji wa mtaguso unavyokwenda polepole. Wengine wameshughulikia miundo tu ya Kanisa, bila ya kujali fumbo la Kimungu lililomo ndani yake. Pengine umekosekana upambanuzi, k.mf. wengi walipofuata mitazamo ya ulimwengu uliomuasi Mungu badala ya kujadiliana nao ili kuuokoa.

Matatizo yaliyojitokeza baada ya mtaguso yanaonyesha haja ya kuupokea vizuri zaidi, kwa kupiga hatua nne zifuatazo:

1. Hati za mtaguso zijulikane na watu wengi zaidi na kwa dhati zaidi.

2. Zipokewe kwa moyo.

3. Zizingatiwe kwa upendo.

4. Zitekelezwe maishani.



NAMNA YA KUELEWA MTAGUSO edit

Tukitaka kuelewa vizuri hati za mtaguso, ni lazima tuzizingatie zote 16 zilivyo na zinavyofungamana. Ni lazima pia tutie maanani hasa katiba zake 4, kwa kuwa ndizo hati kuu zinazotuwezesha kuelewa maagizo 9 na matamko 3. Tena hatutakiwi kutenganisha mtazamo wa kichungaji na msingi wa imani wa hati hizo, wala kutenganisha roho ya mtaguso na hati zenyewe. Mwishowe mtaguso ueleweke katika mapokeo ya Kanisa kwa kuwa katika mitaguso yote Kanisa ni lilelile. Hivyo tu tutapata mwanga tunaouhitaji kwa wakati huu.

Tahadhari hizo zote zinahitajika kwa sababu katika kutekeleza mtaguso yamejitokeza maelekeo mawili ambayo yanapingana na kuvuruga hali ya Kanisa. La kwanza linadai mabadiliko yasiyolingana na mtaguso, ingawa wenyewe wanasema ni maendeleo yanayotakiwa na roho ya mtaguso. Maendeleo ya namna hiyo hayakubaliki kwa sababu hayajali mapokeo ya mitume yanayodai imani idumu kuwa ileile. La pili linaambatana na mambo ya zamani, bila ya kujali ishara za nyakati zetu zinazodai mambo mapya pia kwa wokovu wa watu wa leo na wa kesho.

Ni wajibu wa maaskofu chini ya papa kutambua yapi yanajenga na yapi yanazuia ujenzi au pengine yanabomoa Kanisa. Ndiyo kazi inayofanyika hasa katika sinodi (= pamoja-njia, yaani kusafiri pamoja). Kati ya sinodi za ngazi mbalimbali kuanzia ile ya jimbo, muhimu zaidi ni zile za kimataifa zinazofanyika mara kwa mara huko Roma (mtaa wa Vatikano), zikikusanya maaskofu wawakilishi wa nchi zote na baadhi ya wakuu wa mashirika ya kitawa.



JUHUDI ZA KUTEKELEZA MTAGUSO edit

Kama vile mitaguso mikuu iliyotangulia kupanga urekebisho wa hali ya Kanisa, mtaguso wa pili wa Vatikano pia ujumbe wake hautaweza kuzaa matunda isipokuwa kwa juhudi za muda mrefu. Miaka ishirini baada ya mtaguso kumalizika, sinodi maalumu iliyoitishwa ili kutathmini matokeo yake ilisema wazi kuwa kazi bado sana, kwa namna ya pekee kuhusu kulenga utakatifu kwa waamini wote. Ndiyo maana ilihamasisha tufanye juu chini ili ujumbe wa mtaguso usikilizwe upya katika kila jimbo. Ni lazima tushike jembe kwa kazi hiyo bila ya kuangalia nyuma tukipatwa na matatizo yasiyoepukika.